
Mwenyekiti wa chama cha upinzani nchini Tanzania Chadema amesema kama chama hawana imani na watendaji wa mahakama licha ya kwamba wanaiheshimu kama "muhimili muhimu wa taifa ."
Bw Freeman Mbowe ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho ametolea mfano hukumu ya kufungwa jela miezi mitano aliyopewa Mbunge wa chama hicho Joseph Mbilinyi ''Sugu'' anasema mahakama ilishinikizwa kutoa hukumu hiyo.
Mwanasiasa huyo pia amevituhumu vyombo vya dola akisema vimekuwa vikishiriki katika kupanga na kutekeleza mashambulizi mbalimbali ya kudhoofisha demokrasia nchini Tanzania.
Akiongea na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho, Bw Mbowe alitolea mfano tukio la hivi karibuni la jeshi la Polisi kutumia risasi za moto kuwakabili waandamanaji wanachama wa chama hicho ambao "hawakuwa na silaha za aina yoyote."
Mbowe aliyekuwa amaembatana na viongozi wengine wa juu wa chama hicho amesema wanaungana na Chama cha Wananchi CUF kuituhumu tume ya taifa ya Uchaguzi NEC pamoja na ZEC katika kupindisha uchaguzi na kuchochea uchaguzi usio wa haki.
Baada ya mkutano huo, Bw Mbowe na wenzake sita waliitika wito wa jeshi la polisi na kwenda kuripoti polisi.
Walikuwa wakikubali wito waliopewa siku za hivi karibuni baada ya uchaguzi mdogo katika Jimbo la Kinondoni uliopelekea maandamano yaliyosababisha kifo cha mwanafunzi wa chuo kikuu Akwilina Akwiline.
Watanzania wanasemaje kuhusu kufungwa kwa Joseph Mbilinyi?
Hatua ya kufungwa jela kwa Bw Mbilinyi na Katibu wa Chadema Kanda ya nyanda za juu kusini, Emmanuel Masonga imepokelewa na baadhi ya Watanzania mtandaoni kwa mshangao.
Baadhi, kama vile Evarist Chahali wametazama hiyo kama ishara ya dalili za utawala wa kiimla.
Oraibtz naye ameandika kwamba: "Huwezi kupendwa ukimfunga Sugu"
Richard Mbalala naye alitumia lakabu yake mbunge huyo, 'Sugu' kutoa maoni yake na kusema: "Ukisugua sugu, sugu zinakuwa sugu zaidi."
Visa vya mauaji ya kutoweka kwa watu Tanzania
- Mauaji ya Kibiti mwaka 2017: Viongozi wa CCM, askari zaidi ya 10 na wananchi karibu 40 katika eneo la Kibiti walishambuliwa na kuuawa na watu wasiojulikana.
- 11 Februari, 2018 Kiongozi wa Chadema Daniel John alitekwa na kisha aliuwawa kikatili wakati wa Kampeni za Uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni. Mwili wake ulipatikana mnamo 14 Februari.
- Mnamo 7 Septemba, 2017, Mnadhimu Mkuu wa upinzani bungeni, mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu alipigwa risasi na watu wasiojulikana katika eneo la Area D Mkoani Dodoma. Bw Lissu pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika.
- 21 Novemba, 2017 Mwandishi wa habari wa Mwananchi Communications Limited Azory Gwanda alipotea katika mazingira ya kutatanisha na mpaka sasa hajapatikana.
- Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema Ben Saanane alipotea katika mazingira ya kutatanisha.
No comments:
Post a Comment