Usipitwe na hizi...


Saturday, 3 March 2018

28,000 mnada wa Pugu wakalia kuti kavu



WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ameunda timu ya wataalamu ili kuhakiki uhalali wa nyaraka za wananchi wapatao 28,000 wanaioshi ndani ya eneo na Mnada wa Mifugo wa Kimataifa wa Pugu uliopo Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam ili kuiwezesha serikali kufanya maamuzi sahihi ya kumaliza mgogoro huo uliodumu kwa miaka mingi sasa.
Alimuagiza Katibu Mkuu Mifugo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Maria Mashingo kufanya tathmini hiyo ndani ya mwezi mmoja na kupita katika Kaya zote 5,700 zinazoishi ndani ya eneo la mnada ili kuiwezesha serikali kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro huo uliodumu kwa miaka mingi sasa.
Akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Bangulo, Pugu Stesheni jana, Waziri Mpina alisema mgogoro huo unafahamika katika ngazi zote kuanzia wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi hivyo ni lazima kama viongozi waliopewa dhamana kuhakikisha suala hilo linafika mwisho tofauti ilivyo sasa ambapo wananchi wamekuwa wakiishi kwa hofu kila siku.
Aliwaomba wananchi hao wa Bangulo kuwa watulivu katika kipindi hiki cha mwezi mmoja cha kufanyika tathmini hiyo na kuwataka watoe ushirikiano wa kutosha kwa timu hiyo itakayokwenda kufanya tathmini ili kuiwezesha serikali kufanya maamuzi sahihi yatakayozingatia misingi ya haki kwa pande zote zinazosigana katika mgogoro huo.
Kufuatia hali hiyo Waziri Mpina aliwataka wananchi wote wanaoishi ndani ya eneo la mnada kutofanya shughuli zozote za kuendeleza makazi yao hadi hapo tathmini hiyo itakapokamilika na kuwasihi kuendelea kuishi kwa amani bila kuwepo na mifarakano yoyote na wadau wengine wanaotumia huduma za mnada huo.
Alisema Hati ya Ardhi inatolewa kwa mujibu wa sheria hivyo mtendaji yeyote wa serikali aliyediriki kutoa hati wakati akitambua eneo hilo la mnada lina hati yake ni kinyume cha sheria na hivyo ni lazima wahusika wote walioshiriki kuhalalisha uvamizi huo watachukuliwa hatua za kisheria.
Mkuu wa Mnada wa Pugu, Kilambo Samweli alisema katika ukaguzi huo mfanyabiashara mmoja alikuwa na kibali cha kubeba mbuzi 116 lakini baada ya uhakiki ulioongozwa na Waziri Mpina ilibainika kuwa na mbuzi 228, hivyo kuamriwa kulipa Sh 836,000 kama mapato ya Serikali. Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara alimshukuru Waziri Mpina kufika katika eneo hilo na kuwaomba wananchi kuendelea kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha kufanyika tathmini hiyo ili ukweli uweze kufahamika.

No comments:

Post a Comment

Pages