Usipitwe na hizi...


Wednesday, 7 March 2018

SIMULIZI YA KWELI NILIONGEA NA SHETANI ILI NIWE TAJIRI

Image result for simulizi ya kweli niliongea na shetani 7
SIMULIZI YA KWELI: NILIONGEA NA SHETANI ILI NIWE TAJIRI
MTUNZI: STALLONE JOYFULLY
SEHEMU YA SABA
Chini ya matiti yangu, mara mgongoni.
Kucha pekee hazikutosha. Nikajipeleka ukutani. Najikuna
lakini wapi. Muwasho ukazidi. Nikaendelea kuwashwa
zaidi. Muda wote huo sikushituka mapema kama nilikuwa
sioni kitu chochote. Sikujuwa kama macho yangu
yalikuwa yamefumba. Sikujuwa kama nilikuwa nikitembea
kwenye giza nene.
"nimekuwa kipofu" nilijiuliza kwa uoga. nikapapasa
ukutani kwa shida na kulitwaa taulo langu. Nikajifunga
mpaka eneo la kifua na kulifanya liwe fupi kidogo. hapo
hapo nikausikia mguso wa mkono ukiugusa mgogo
wangu. Niliuputa ule mkono kwa uoga na kugundua
ulikuwa ni mkono wa mnyama. Mkono ulikuwa na
manyoya manyoya kila sehemu. Nilipiga kelele za kuomba
msaada "baba nakufaaa" sauti yangu haikufika popote
kumbe aikuwa ni babu. Nilimgundua ni yeye baada ya
kunitibu na kupata kuona tena. Alinitibu kwa kunishika
macho yangu huku akiongea maneno Fulani ambayo
sikuyaelewa kwa urahisi. Alikuwa akiyafikicha fikicha
baada ya kupaka mate kiganja chake. baada ya kufumbua
macho, niliona mwanga mkali sana. Kisha ukapotea. babu
aliniuliza. "umefanya nini?"
sikumuelewa babu alimaanisaha nini hivyo ilinibidi
nimuulize. "babu kuna nini?"
babu hakunijibu chochote. Aliniangalia kwa huzuni kisha
linionesha kwa kidole chake katika kioo. Ilikuwa ni taswira
ya Gamboshi. Hapa alinionesha ile siku ambayo nilikuwa
nikikabidhiwa mamlaka yake. Yule kiumbe wa ajabu
alikuwa akinipa masharti ya kuyafuata.
"hakikisha maji hayagusi mwili wako, iwe ya mvua ama
ya bomba. Iwe hivyo kwa muda wa siku tatu" hapo
nikalijua kosa langu. Sikuongea chochote mbele ya babu.
Nilitazama chini kwa aibu. babu aliniuliza tena. "Bella
kama hukuwa tayari, kwanini ulikubali kupewa masharti
haya?" nililia "babu nisamehe" babu alinikatisha kwa sauti
ya ukali "nikusamehe? Nikusamehe vipi?" alikuwa
amekasirika sana. kadiri babu alivyokuwa amekasirika,
ndipo alikuwa akiongezeka urefu. Alikuwa mrefu.
Akaongezeka zaidi. Alikuwa mrefu kupitiliza hata unyayo
wa miguu yake tu, ndiyo iliyobaki bafuni. Vidole vyake
vikagusa bati na kulitoboa kabisa. Kisha alirudi kwa
nguvu za ajabu. Alikuwa akitoa moto alipokuwa akirudi
katika hali yake ya kawaida. Alikua kama yule muhusika
wa kwenye filamu ya ghost rider. akaniambia kwa sauti
iliyotetemeka "umeniuzi sana, umemuuzi mkuu. Siwezi
kusema nimekusamehe ikiwa sio mimi niliyekupa yale
masharti." hapo akaacha kuongea kwanza. Alikohoa,
akakohoa sana kama aliyepaliwa na chakula. Akaniambia
"acha niende. Nimekuja kukuponya upofu ulioupata ili
uende katika msiba wangu ukawaonye wasiuombee mwili
wangu" aliniangalia kwa huzuni kisha aliniambia "Bella
una kazi ngumu na adhabu kali mbele za mkuu" babu
alitoweka kisha akauacha moshi mzito sana bafuni.
Sikuoga tena Nilitoka bafuni na kurudi chumbani. Nilivaa
nguo za kawaida tu ndani kisha nilijitanda kanga mbili za
aina moja. Hatimaye nilitoka kulekea msibani. eneo la
msiba lilifurika watu wengi na kujaa simanzi nzito. Rafiki
zake babu walikuwepo ndugu na wengine ambao
sikuwafahamu, wote walikuwa wana huzuni kubwa. Ndugu
waliponiona walilia kwa sauti ya juu sana. Naweza
kusema kwa upande wa baba yangu mzazi, babu
alinipenda sana mimi kuliko hata watoto wake aliowazaa.
Alinipenda kuliko kitu chochote au mtu yeyote. Hakuna
mtu ambaye alikuwa hajui kwamba babu alikuwa
ananipenda kiasi kile. Tuliingia chumbani ilipo maiti ya
babu ikioshwa.
shangazi mkubwa aliyebaki, akasema "hajafa katika
mapenzi ya mungu. Hapa kuna jambo. Inabidi tumuite
mchungaji kabla hajazikwa" mimi niliogopa sana. Sauti ya
babu ikajirudi kichwani mwangu kama mwangwi.
"hakikisha mwili wangu hauombewi" Nikapata nguvu ya
kuzungumza "hapana shangazi. Huyu asiombewe wala
kuagwa ninaomba iwe hivyo"
sikuwa na hakika kama shangazi angekubali kile
nilichomueleza kwa sababu aliniangalia kwa jicho kali
sana kisha alisema. "Bella!?" alinishangaa kwa tuo. Mimi
macho yalinitoka nisijue nitafanya nini akaendelea.
"kwanini hutaki babu yako asiombewe, wala kuagwa?"
Nilijua ni lazima mtu yeyote angeuliza swali kama hilo.
Mtu yeyote mwenye akili timamu, angeniona kama
niliyeanza kurukwa na akili. Hivyo nikashikwa koo na
kigugumizi cha ghafla. Kigugumizi nisijue nitajibu nini? Si
shangazi pekee aliyeshangazwa na jambo hilo! Hata mimi
pia sikuelewa nilipoambiwa kwa mara ya kwanza. Mimi
pia nilijiuliza sana, kwanini mwili wa babu usiagwe wala
kuombewa?. "mimi sijafa katika mpango sahihi, Hivyo
katika kuagwa huko, kuna watu ambao wanaweza kutoa
siri kuwa mimi sijafa na sipo katika lile jeneza"
nikaikumbuka sauti ya babu. Nilichoambulia kukifahamu
kutoka kwa wachawi, yaani wanapoua mtu kabla siku
zake za kufa hazijafika, basi humchukuwa na kwenda
kumuhifadhi sehemu ambayo humtumikisha kazi nyingi
sana. Kama vile kulima shamba kubwa sana, ambalo
huchosha hata kikundi Kikubwa cha watu lakini msukule
mmoja hulima ndani ya dakika chache. Hubeba mizigo ya
wachawi au kwenda kuleta damu, baada ya kusababisha
ajali katika barabara kuu iendayo mikoani. Na pale katika
jeneza wanaweka mgomba ambao humuwakilisha yule
mtu ambaye amechukuliwa msukule. Watu ambao
hawana uwezo wa kichawi hawawezi kugundua kama ule
ni mgomba. Bali mchawi pekee au mwenye nguvu kweli
za kimungu. Wazazi ndugu jamaa na marafiki zake
marehemu, Wanaweza hata kulia kwa kumshika mshika
kwa huzuni, lakini wasione tofauti yeyote na mwili wa
kawaida. Ila kwa babu hakuwa msukule. Babu alikufa ili
kwenda kuitumikia Gamboshi baada ya mkataba
walioafikiana kutimia. Hivyo alikuwa analipa fadhila.
Fadhila ya kipumbavu, fadhila ya kijinga, fadhila ya
kishenzi kutoa uhai wako kwenda kuishi katika mji wa
kichawi Gamboshi.
Nilipokuwa katika kuwaza nisijue nini nimjibu shangazi.
Ghafla mbele yangu nilimuona babu. Babu alikuwa
akitabasamu. Aliniambia "usijali nitakusaidia" Kisha
alipotea.
nilimgeukia shangazi mara baada ya tukio hilo la
kushitukiza. Nikataka nimjibu, akaniambia huku
akitabasamu. "Bella umeanza kuwa na akili sana
mwanangu" alinishika shika kichwani na kutabasamu kwa
raha. Nilijiuliza shangazi alikuwa akimaanisha nini?
Nilibaki katika bumbuwazi ya ajabu, nisijue nini shangazi
alimaanisha. Aliendelea "basi nitapinga mwili wa babu
yako usiagwe wala kuombewa, ila ni ngumu sana
kueleweka kwa watu timamu"
nilishangaa sana. Kukubali huko kwa shangazi. Lilikuwa ni
jambo la haraka, wakati mimi sikujibu chochote!
Kulinifanya nijiulize maswali mengi. 'babu alitumia kinywa
changu kumjibu shangazi, bila mimi kufahamu? Alimfunga
akili shangazi hata asikumbuke kuwa hilo ni jambo la
kushangaza? Mwili usiagwe wala kuombewa? Ni ajabu na
inayoshangaza?'
mshituko wangu haukuwa na madhara yoyote kwa
shangazi. Hakuniuliza jambo lolote, tukatoka chumba cha
kuoshea maiti ya babu. Ndugu waliokuwa wakisubiriwa
kutoka katika kila pande ya visiwa vya ukerewe. Visiwa
ambavyo babu ndipo alipozaliwa, walikwishafika baada ya
siku tano za msiba baadaye. Shangazi aliwaeleza
nilichomueleza. "naona ni vyema tukamsikiliza kama
alivyosema" nilishangazwa na kaka zake babu,
walivyounga mkono hilo jambo. Ila mmoja aliweka
pingamizi. Hapo ndipo palinigusa, nikataka nifahamu. "ila
nyinyi jamani mbona tunataka tuishangaze jamii?"
alikuwa ni shangazi aliyemfuata yule niliyekutana naye
kule Gamboshi, kuzaliwa. Ndugu wa baba niliwafahamu
kutokana na babu kunitambulisha kwa sauti ya kawaida
bila mtu yeyote kusikia. Babu alikuwa eneo hilo la msiba
bila mtu yeyote kumuona. "wewe dada Suzi embu
nyamaza. Wewe ufahamu kuwa Bella ndiye mrithi wa
mizimu ya ukoo wetu?" nilipigwa na butwaa. Hata hawa
walifahamu kuwa mimi tayari nimekwisha zuru
Gamboshi? Yule aliyemnyamazisha shangazi Suzi,
alinigeukia na kuniambia. "mwanangu sawa tumekuelewa.
Usijali kuhusu hilo, tutafuata kila ulichotuelekeza." kikao
cha familia kikavunjwa baada ya lile nililoliongea
kupitishwa bila kupingwa zaidi. Msiba ulienda kimipango
bila kuvunjika hata moja. Babu akazikwa katika makaburi
ya kigogo mburahati.
.........................................
Baada ya msiba, ndugu wa baba ambao hatukuwahi
kuonana kabisa walijitambulisha kwangu na mimi kwao.
Wengi walipendezwa sana kuniona na mimi sikuzificha
hisia zangu kuwa pamoja nao. Nilifurahi sana. Shughuli
nyingine zikaendelea. Siku moja mimi na baba mkubwa
Christopha tulikuwa nje ya nyumba chini ya mti wa
mchikichi tukizungumza.
Baba mkubwa aliniuliza "sasa Bella ilikuwaje ukavunja
masharti?" kikohozi kikavu kikanipitia. Nilikohoa sana
kabla sijamjibu lolote, aliniambia tena."unafahamu sababu
ya kifo cha babu yako?" nilimjibu kwa wasiwasi. Hii
ilitokana na kudhani kuwa huenda kuwa sababu ya kifo
chake ilikuwa ni siri yangu pekee yangu. Nilimwambia
"hapana sifahamu baba" nilinyamaza kidogo kumeza
mate kisha niliongeza "ninachofahamu ni kifo cha ugonjwa
wa ghafla tu. Nadhani inaweza ikawa ni uzee?" nilijitia
kuuliza swali ili nimchimbe alichotaka kunieleza.
aliniamba yote yaliyohusu kifo cha babu yangu. "babu
yako amejitoa kafara baada ya wewe kushindwa
masharti. Kifo chake kimesababishwa na wewe.
Hakustahili kufa, ila wewe" mshangao ulikuwa wazi katika
macho yangu na uso wangu. Midomo yangu ilitetemeka
sana kwa uoga. Nikamuuliza. "nahisi sijakuelewa baba?"
alitabasamu kwa kejeli na kuniambia "ulipopewa masharti
yale matatu na ukashindwa kutimiza, babu yako
aliambiwa kuwa baada ya siku tatu ungekufa, ungekufa
kinyama. Ndipo alipobatilisha adhabu hiyo na kuongea na
mkuu wake na kuomba adhabu hiyo apewe yeye." bado
nilikuwa nikishangaa nisijue chochote anachonieleza kati
ya hivyo. Nilikuwa gizani, hata babu alinificha. Sikujua
sababu ya babu kunificha jambo kama hilo.
baba mkubwa alinieleza jambo lingine "umewahi kujiuliza
kwanini babu yako hutoka machozi ya damu kila
alipokuwa akikutokea?" macho yangu yakapata nuru ya
ajabu na kuwa na shahuku ya kutaka kujua sababu.
Jambo hilo la machozi ya damu lilinichanganya sana.
Nilijibu kwa shahuku ili nifahamu ilikuwa inasababishwa
na nini. "hapana sifahamu. kwanini alikuwa anatoa
machozi ya damu?" akaniambia "inatokana na..."
ghafla sauti yake ikaishia mdomoni kwake. Nadhani hata
masikio yake mwenyewe hayakuisikia sauti yake vyema.
Hili likanishangaza. Nikamuuliza "baba una nini?"
macho yalinitoka kwa uoga. Yeye alikuwa akijitahidi
kupiga kelele lakini sauti haikutoka. Nilitoa mbio
tulipokuwa tumekaa na kwenda kuwaita ndugu zetu
wengine. Walipofika tulipokuwa tumekaa, baba mkubwa
hakuwepo. Nilishituka sana. Shangazi Suzi aliniuliza
"we Bella! Yuko wapi sasa?" kwa kuwa bado sikuelewa
kilichotokea, niliwaeleza kwa kunyoosha kidole. Mara
nikaipata sauti yangu "alikuu..wa alikuwa hapa jamani"
kila mtu alikuwa katika hali ya kutaharuki asijue nini
kimetokea. "kwani mlikuwa mnazungumza nini na nini
kilitokea" Shangazi Suzi aliniuliza "tulikuwa tumekaa hapa
na yeye alikuwa ananieleza sababu ya kifo cha babu"
kabla sijamaliza kuongea, sauti ya babu ikasikika
masikioni mwangu. "usimueleze yeyote kuhusu ulilosikia"
nilipokuwa nikiitafakari ile sauti. Yule shangazi mkubwa,
aliniuliza "bella una nini? Mbona umenyamaza" Nilimjibu
yule shangazi "alikuwa akinieleza jinsi ambavyo babu
alikuwa akinipenda sana. Alinieleza ambavyo baba yangu
mzazi alikuwa ni mtu wa watu na kifo chake kilisikitisha
wengi"
Ilibidi nidanganye. wengine walifahamu hila zangu na
kuondoka nilipo. Mimi mahali pale nikabaki nikiwa na
shangazi mkubwa na Suzi, wakinidadisi hili na lile. Macho
yangu muda mwingi yalikuwa yakiangalia juu ya mchikichi
huenda angekuwa amebebwa na babu, lakini hakuepo.
Nikatazama njia ielekeayo barabarani labda nilidhani
angekuwa akija, napo kukawa patupu. Wote tukaingia
ndani kwa kuwa tayari ilikuwa jioni. tukiwa tunasimuliana
hadithi mbalimbali, tulishituswa na sauti ya uoga aliyoitoa
shangazi Suzi. Shangazi alikuwa ameenda chooni. Hivyo
alitoka mbio mpaka sebuleni tulipo sisi. Alikuwa na jasho
jingi usoni na uoga uliujaza uso wake. "kuna nini?" baba
mdogo Joseph, alimuliza shangazi. Shangazi alikuwa
ametoka chooni, chupi ikiwa chini, sketi akiwa
ameishusha kama kawaida, macho kayatoa pima. Bila
shaka yale maji maji niliyoyaona yakichuruzika miguuni,
ulikuwa ni mkojo uliomtoka ghafla. Wachache tukamcheka
kwa kuwa shangazi huyu, ndiye alionekana kuwa mtundu
katika familia yote ya watoto wa Babu. "nimekutana na
James chooni" alizungumza macho kayatoa isivyo
kawaida. Alikuwa akituangalia sisi kisha akigeuka
akiitazama njia ielekeayo choooni. Wote kwa pamoja
tukaanza kushituka na kukaa kwa uoga. Wachache
tulisimama kama tulikuwa na ujasiri wa kuelekea chooni
vile.
shangazi mkubwa akauvunja ukimya "chooni?" ghafla
kicheko cha baba mkubwa James, kikasikika kikija eneo la
sebuleni. Nilimshuhudia shangazi Suzi akitaka kukimbia,
lakini kukawa hakuna njia zaidi ya kuelekea popote. Hivyo
akawa akiwasukuma ndugu wengine. Alikuwa baba
mkubwa James mwenyewe. Alikuwa kama vile ambavyo
nilikuwa naye mchana. Alikuwa akitabasamu kama
hakuna lolote lilitokea. Alinitazama kwa furaha na
kuwaangalia wengine zamu kwa zamu. Kila mtu
alishangaa kwa kujiuliza maswali kadha wa kadha.
Maswali ambayo yalijionesha dhahiri juu ya nyuso zao.
Hakuna ambaye alipata ujasiri wa kumsogelea wala
kuongea naye chochote. Ni mimi peke yangu nilitoka
nyuma ya shangazi yule mkubwa na kumfuata baba
mkubwa Nilimuuliza. "baba mkubwa" kabla sijaendelea
kuongea chochote, aliniziba mdomo na kuniambia
ninyamaze. Alikuwa akitabasamu, hakika alitabasamu kwa
furaha. Baba mkubwa, alizungumza sasa "kwanini
mnaniogopa sasa?" nilimsikia yule shangazi mkubwa
akicheka. Naye alitoka alipo na kumsogelea baba
mkubwa. Alimuuliza "hivi wewe James" hawa walipishana
kuzaliwa. Alianza Shangazi kisha Baba mkubwa james.
shangazi akaendelea "huoni hata mdogo wako ametoka
na chupi chooni kwa uoga?" alikuwa akimuoneshea
Shangazi Suzi. Kwa kweli hakuna ambaye alijizuia
kucheka siku hiyo. Tena walicheka kwa nguvu hata
shangazi akaona aibu. Nadhani hata yeye mwenyewe
hakujijua kuwa chupi ipo chini. Aliivaa haraka haraka
kisha shangazi mkubwa aliendelea "ulikuwa wapi?" baba
mkubwa James akacheka, kisha alisema. "nilikuwa
chooni, kwani nimetokea wapi?" nikauliza ghafla
"umewazaje kuongea tena? Kila mtu akashangaa
"kuongea?"walinyamaza kwa pamoja. Nilipowatazama,
shangazi Suzi aliuliza "kwani alikuwa haongei huyu?"
baba mkubwa James alinishika mkono wangu kisha
alinibinya binya ninyamaze kuongea na kuwaeleza "wakati
nipo na Bella pale chini ya mti nilikabwa na tunda ambalo
nilimeza mbegu zake, sasa ndipo alipokuja kuwaita ninyi
na mimi nikawa nimetoka kuelekea chooni" kila mtu
alicheka kwa kuudhika. Shangazi mkubwa akasema.
"wewe James usitufanye sisi wajinga. Ni masaa mawili
yamepita sasa, tangu wakati ambao hujaonekana. chooni
kote tumekutafuta, mpaka chini ya uvungu hukuonekana.
Sasa huko chooni ulienda choo kipi" shangazi aliuliza kwa
ukali kidogo.
ITAENDELEA!!!

No comments:

Post a Comment

Pages